FALSAFA



Falsafa ni nini?
Falsafa ni juhudi ya kuuliza, kufahamu na kujibu maswali sugu kwa tafakuri.

FALSAFA YA KIAFRIKA NA YA ULAYA

FALSAFA YA KIAFRIKA
Inaweza kugawanywa katika sehemu zifuatazo mbili. Yani, falsafa ya Kiafrika ni aidha
Kiujumla: Falsafa yoyote ile ambayo itaguzia maudhui ya kiafrika au itatumia mbinu za kiafrika kukidhi madhumuni yake.
Kimaalum: Falsafa ile tu imetokana na mtu ambaye ni Mwafrika au an uzao wa Kiafrika.
Falsafa ya Kiafrika inachukua daraja tatu

1. Uhenga-tamaduni: Weledi wa mambo yote ya mila ya watu wa jamii fulani.
Hapa kuna
Falsafa-tamaduni: Weledi wa mila na desturi za jamii na unamilikiwa na watu wote wa jamii hiyo ila, wazee ni wahenga zaidi kuliko watoto.
Falfasa-uhenga: Weledi wa mambo ya mila na tamaduni za jamii zilizomo kwenye mhenga mmoja mashauri.
Falsafa-shehe: Mweledi wa mambo ya mila na tamaduni za jamii pamoja na mambo mengi ya malimwengu

2. Falsafa-itikadi: Uanzilishi ama uzinduzi wa mfumo wa fikira wa kufuatwa na wananchi wote. Hii ilitokana na mataifa ya Afrika kujinasua kutoka kwa ukoloni. Waanzilishi wa mataifa kama Mwalimu Nyerere, Kwame Nkuruma na Leopold senghor walikuwa na maono thabiti ya kuelekeza mataifa yao.

3. Falsafa-taaluma: misimamo zinazotolewa na wafalsafa ambao wanayaandika kinagaubaga k.m. Ngugi wa Thiong’o (kukomboa ubongo)


Maono-mlimwengu ya falsafa ya kiafrika huchukua mfumo:
MUNGU (MIUNGU)—MAPEPO---BINADAMU—VITU HAI---VITU VISIYO NA UHAI

FALSAFA YA ULAYA
Inaanzia na ile ya Wayunani hadi wafalsafa wa siku hizi. Ina historia ndefu kushinda ile ya kiafrika kwa sababu walianza kuandika mambo yao zamani na kuwaza kuziifadhi hati hizo vyema.

MATAWI YA FALFASA
Falsafa inagawanyika kwa matawi tanu maalum

1. Asilia: Ni fani ambayo inatafuta asili ya vitu ama mambo zaidi kuliko na halisi yao.
Inajumlisha vitu vyote ulimwenguni pamoja na malimwengu. Inauliza maswali kama:
Dunia /ulimwengu upo kweli? Je Mungu yupo? Tukikufa mioyo zetu huenda wapi?

2. Ufahamu: Ni somo linalohusu ‘fahamu’. Linazingatia maswali kama:
Naweza kujua nini? Ufahamu unapatikana vipi? Ukweli unadhibitishwaje?
Matawi ya Ufahamu
i) Taamuli- kutambua mambo kwa kutumia akili
ii) Hisia- kutambua mambo kwa kutumia viungo vya mwili yani macho, masikio, pua, mikono na ulimi.

3. Thamani:
A. Sanaa: Maswala kuhusu urembo, nakshi, (ma)umbo na urari.
B. Maadili: Maswala kuhusu jinsi binadamu anastahili kutekeleza mambo. Ina sehemu tanu zifuatazo
i) Asili ya maadili: Maswali yake makuu ni- Je, maadili kweli yako? Yanatoka wapi? Nini kizingatiwe wakati wa kuamua jambo ni nzuri au baya? Na je, kuna kitu kama tabia nzuri?
ii)Msingi wa maadili: Maswali yake makuu ni- Tutafikiaje kiwango kizuri cha kutathmini maadili kama vile amri kuu ‘tendea mwenzako jinsi ungependa wewe utendewe’
iii)Maadili ya utendakazi: Maadili katika taaluma mbali mbali kwa mfano- Wanasheria, Wanahabari, Madaktari n.k.
iv)Saikolojia ya utu: Inashuhudia swala kama- Umri wa kuwajibika kwa watoto
v)Maadili ya dharura: (Maadili huru) Inashuhudia jinsi watu wanavyokabiliana na juhudi zao kila siku na hivyo jinsi maadili yao yanavyodhihirika yenyewe.

4. Dabiri: Jinsi ya kurazini vyema. Inatumiwa na wanafalsafa kutafuta na kudhibitisha ukweli katika mambo yote. Inajumlisha mambo kama nususi na ukimu. Taratibu zake mbili ni:
i) Kutohoa: Inazingatia kutafuta ukweli mahususi kutoka na ukweli pana uliopo
k.m.
(kama)     binadamu wote wana uhai
(na pia)    Kamau ni binadamu
(hatima yake basi)        Kamau ana uhai
ii) Kulimbikiza: Inazingatia kutafuta ukweli pana kutoka kwa ukweli mahususi uliopo.
k.m.
(kama)    Kamau ana uhai
(kama)   Omondi ana uhai
(na pia)  Kamau na Omondi wote ni binadamu
(hatima yake basi)     Binadamu wote wana uhai

* Matawi haya manne yanatengemeana kwa kufanikisha jukumu zao. Bila ufahamu hakuna jambo linalowezaeleweka; na, kueleweka, lazima chanzo na kiini cha kitu hicho kijulikane; kiini cha kitu hakiwezijulikana bila maswali sugu kuulizwa na majibu ibuka kupigwa tarubini kwa dabiri; lakini, dabiri haiwezifanywa kwa ukamilifu bila kuzingatia maadili; nayo, maadili lazima yadhibitishwe kwanza yapo (kwa kutegemea falsafa asilia)na yana msingi(kwa kutegemea ufahamu).

5. Siasa: Jinsi ya kutawala vyema

NUSUSI KUHUSU FALSAFA
1.  Falsafa sio somo maalum ila ni mbinu katika masomo au fani zozote kwa ujumla. Pia inawezasemwa kuwa ni kitovu cha usomi wote.
2. Falsafa inalenga sana maswali kuliko majibu. Kwa hivyo hata jibu likitolewa falsafa itauliza kama jibu hilo ni la kweli au la.
3. Falsafa hubadilika baada ya muda fulani kulingana na mambo yanaowakabili watu katika enzi yao na pia mahali ambapo inafanywa kwa mfano: sokoni, makanisani, vyuoni, kwenye migongamano na, katika mtandao  

UMHIMU WA KUSOMA FALSAFA
1. Falsafa inatusukuma kuwaza kwa undani kuhusu mambo yote hata yale tunayoyachukulia kuwa kawaida.
2. Ina faida katika taaluma nyingi kama vile uanasheria, usamamizi, uanahabari, utafiti na udaktari ambapo kufikiri kwa undani zaidi na kupata majawabu yasiyo bayana kwa watu wote.
3. Ina faida katika kazi nyingi kwa sababu hutoa mwelekezo thabiti kwa mambo ya maadili
4. Falsafa ni somo pana kwa hivyo humpa mtu (mwanafunzi au mtaalam) ujuzi na fikira pana na kuwafanya kuwa watetezi na wahudumu wema zaidi
5. Pia huwapatia watu mbinu za kufanya utafiti bora na tena kunoga ujuzi wa kujadili, kuchambua, kuzingatia misimamo tofauti na kurasimu mawasiliano yao
6. Falsafa inakusaidia kuwa binadamu bora ambaye anachangia kikamilifu kwa uwezo wake wote wa kielimu.
* Falsafa si fani/ kazi ya watu wa kale tu, au wanachuoni na wataalam maalum ila inafaa kuwa juhudi ya watu wote katika harakati ya kuboresha maisha ya wote. Maswali kama, ni nini kizuri, nini kibaya, nini kinastahili, na nini hakistahili hayawezi kuwachiwa watu wachache tu.

Maoni

Chapisha Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

IKTISADI

Katiba kwenye mtazamo wa miraba tatu (Sehemu II-I): Kugeuza katiba bila Kura ya maoni